Published On: 05-08-2016 07:51:13

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa  Serikali kuhamia Dodoma siyo siasa kama watu wanavyodhani.

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa  akiwa katika picha ya pamoja  na wazee wa Dodoma baada ya kuzungumza na Wazee, viongozi wa dini, wafanyabiashara na wananchi wa Dodoma kwenye ukumbi wa Hazina , Dodoma .

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa  Serikali kuhamia Dodoma siyo siasa kama watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na kwamba serikali imekamilisha  eneo la kisheria  juu ya uhamishaji wa Makao Makuu kuja Dodoma na katika bunge la Septemba sheria hii itapatikana .
Hapa tulipofika ni hatua ya utekelezajiwa pamoja na hakuna namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii sio siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo la sheria juu ya uhamishaji wa Makao Makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii itapitishwa. Alisema
Alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akiongea  na viombozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma, viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa Dini, wajasiliamali, wafanyabishara,wakuu wa taasisi za elimu na watoa huduma mbalimbali katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Waziri Mkuu aliutaka  uongozi wa Mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa serikali wa kuhamia Dodoma. Pia alitoa siku kumi na nne (14) kwa uongozi wa Mkoa wa Dodoma, kukamilisha mpango kazi wao na kukabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye Mpango mkubwa  wa Serikali kuu.
"Uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchiofisi ya Waziri Mkuu  na ofisi ya TAMISEMI isimamie na kuratibu majukumu hayo. Ndani ya siku kumi na nne nipate mapendekezo ya namna mtakavyotekeleza . Naagiza kiundwe kikosi kazi kitakachojumuisha  makundi yote niliyoyataja "Alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema chimbuko la uamuzi wa kuifanyaDodoma  kuwa  Makao Makuu ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa  Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo imeendeea  kudumu katika ilani ya  uchaguzi ya mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151.
“Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa ujumla", alisema.

Akiweka msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili viongozi hao, Waziri Mkuu alisema masuala yanayotakiwa kufanyika kuanzia sasa ni pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha eneo la makazi ya Serikali Kuu litakalotumika kwa ofisi za wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara elimu na taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinakamilika kwa haraka na linakuwa tayari kwa matumizi.

“Natambua kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji jitihada za pamoja. Hivyo kila taasisi na mtu mmoja mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa tunajipanga vizuri na kuweka mazingira ya ujio wa Serikali katika maeneo yote muhimu,” alisema.

Alizitaka Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo mmoja wa upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja, utakuwa wazi usio na urasimu.
“Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta na uuzaji wa viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu kutoka kwa madalali,” alisisitiza.
 
Waziri Mkuu aliwaonya CDA na Manispaa zisibadili ramani ya mipango miji iliyokwishawekwa awali kama vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na akaagiza maeneo hayo yote yarejeshwe na kufufuliwa.

“Natambua katika makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo maalum vijulikanavyo kama D Centers kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Cha ajabu sasa kuna magenge, groceries na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao Makuu haya maeneo sasa yatumike kuwekeza maduka makubwa (shopping malls) ambamo huduma zote mbalimbali hupatikana,” alisema.

Aliitaka Manispaa iboresha usafi wa mazingira na bustani zake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka manispaa ya mji huo ishirikiane na TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na taa za barabarani mji ukae kisasa, na usalama uwe bora zaidi.
“Eneo jingine muhimu ni Manispaa na CDA kuhamisha makundi mbalimbali ya wafanyabiashra na huduma za masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo yaliyo rasmi na bora zaidi. Hii ni pamoja na maeneo ya maegesho ya bajaji, bodaboda, taxi na daladala. Pia mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe, vyoo vya kulipia pia vijengwe katikati ya mji,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa majengo(TBA) waorodheshe majengo yote ya Serikali na taasisi zake yanayotumika kwa sasa na yasiyotumika, “Nataka muyawekee utaratibu maalum wa matumizi yake ili tupate kujua yanayoweza kutumika kwa muda kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii ni pamoja na jengo jipya la Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”
Aliwataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.

CAPITAL DEVEROPMENT AUTHORTY

 Quick Links

Contact Us

Director General
P.O. BOX 913
Dodoma,Tanzania
Tel:   +255 262321569/+255 262324053
Fax:   +255 26 2322650
Email:   info@ cda.go.tz
Website:   www.cda.go.tz

Follow Us On: