Published On: 23-03-2017 20:40:59

Maendeleo Ya Mradi Wa TSCP.

Mkurugenzi Mkuu Wa CDA Mhandisi Paskasi Damian Muragiri.

Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ni miongoni mwa Mamlaka zilizopata ufadhili wa kutekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati unaofadhiliwa na Mkopo wa Benki ya Dunia na msaada kutoka Serikali ya Denmark. Miji mingine iliyopata ufadhili huu ni Jiji la Tanga, Jiji laMwanza, Jiji la Mbeya, Jiji la Arusha, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Manispaa ya Ilemera,Manispaa ya Dodoma ambayo kwa pamoja inaratibiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (PORALG) Akizungumza katika mahojiano maalum Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) Bw. Paskasi Muragili alisema utekelezaji wa mradi wa uboreshaji Miji Tanzania ulianza rasmi mwaka 2011 kwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa na chang’ombe (Km 15.65), Area “A” na Kikuyu (Km 11.47), pamoja na Ujenzi wa Mtaro wa maji ya mvua katika maeneo ya Nkuhungu na Mwangaza (Km7.2) chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu na awamu hii ilikamilika rasmi mwaka 2015. Aliongeza kuwa mji wa Dodoma umejiongezea barabara za kiwango cha lami zenye urefu upatao kilomita 42 (kilomita 27 chini ya usimamizi CDA na kilomita 15 chini ya usimamizi wa Manispaa ya Dodoma). Baada ya Mradi huu kukamilika kwa awamu ya kwanza na kufanyiwa tathmini kulitokea mapungufu yaliyojitokeza ambayo yalipelekea kuongezwa kwa fungu la ziada kwa ajili ya kuboresha miradi ambayo ilikwishakamilika kwa lengo la kukidhi malengo ya mradi. Muragili alisema maboresho hayo yamepelekea kuanza kwa awamu ya pili ya mradi inayoendelea hivi sasa katika maeneo Kisasa, Chang'ombe Area "A" na Kikuyu ambapo inahusisha upanuzi wa barabara za eneo la Kisasa kwa kiwango cha lami, Ujenzi wa njia za watembea kwa miguu eneo la chang’ombe, Uwekaji wa taa za barabarani katika maeneo ya Kisasa na chang’ombe, Ujenzi wa vivuko maji katika maeneo yote, Ujenzi wa mitaro ya maji katika maeneo ya Hijra, Chang’ombe na Kikuyu, Ujenzi wa barabara inayounganisha barabara kuu ya Iringa na Kikuyu pamoja na uimarishaji wa mitaro ya pembezoni mwa barabara. Alisema kuwa sehemu ya Pili ya Mradi ilijikita katika kujenga uwezo wa taasisi kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka juu ya sheria na taratibu za manunuzi iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia, Matumizi ya teknolojia za Kisasa (Mifumo ya Kijiografia, Usanifu), Usimamizi wa mikataba, Ufuatiliaji na tathmini ya miradi, Mbinu za uongozi, Utunzaji wa mazingira na usimamizi wa fedha na matumizi ya mifumo katika ukusanyaji wa mapato. Akifafanua zaidi alisema Mamlaka imeweza kutoa elimu kwa wadau katika masuala ya usalama barabarani, Kujikinga na maambukizi ya Ukimwi,Uhifadhi wa mazingira, uzingatiaji wa taratibu za Mipango Miji, umuhimu wa ulipaji kodi na Utunzajiwa miundombinu lengo likiwa ni kuwashirikisha kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa uendelezaji Miji Tanzania ili kuwajengea uelewa sahihi kuhusu mradi huo. "Mamlaka imeweza kubuni na kuweka mikakati bora ya ukusanyaji wa mapato, huduma za ushauri wa kitaalam kuhusu uboreshaji wa vyanzo vya mapato pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa ulipaji kodi kwa hiari" Alisema Muragili. Aidha alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huu, yapo mafanikio mengi ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya ujenzi na uendelezaji wa maeneo ya Mji hususani yale yaliyopitiwa na Mradi, Ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua umesaidia kupunguza madhara ambayo yangeweza kutokea kwa watu pamoja na hasa katika kipindi cha mvua. Hali kadhalika wananchi na wadau waliopo maeneo ya mradi wameweza kunufaika na mafunzo mbalimbali juu ya matumizi bora ya barabara, uhifadhi wa mazingira na namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi (HIV/AIDS awareness). Alisema kuwa ujenzi wa barabara umechangia kuwepo kwa huduma bora ya usafiri wakati wote katika maeneo husika ambapo kabla ya mradi maeneo mengine yalikuwa hayafikiki. Mahusiano mazuri baina ya Mamlaka na Wadau mbalimbali yameongezeka hasa katika kipindi hiki ambacho mradi huu umesaidia kuondoa kero za muda mrefu za wakazi wa Mji Mkuu. Muragili alieleza matumizi ya mfumo wa kukusanyaji wa mapato umewezesha kuwekwa kwa kumbukumbu sahihi za wateja, utoaji wa hati za madai na risti, kuwatambua wadaiwa na kudhibiti mianya ya wizi. Aidha ametoa wito kwa wananchi kutunza na kuheshimu miundombinu inayojengwa na Mamlaka ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Mji Mkuu hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inahamia Makao Makuu ya Nchi kuja Dodoma.
CAPITAL DEVEROPMENT AUTHORTY

 Quick Links

Contact Us

Director General
P.O. BOX 913
Dodoma,Tanzania
Tel:   +255 262321569/+255 262324053
Fax:   +255 26 2322650
Email:   info@ cda.go.tz
Website:   www.cda.go.tz

Follow Us On: